Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson akishirikiana na wabunge wa Mbeya wameipa timu ya Mbeya City Shilingi 3,000,000 kama motisha kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa mwishoni mwa juma hili.
Makabidhiano hayo yamefanyika mjini Dodoma wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa na Spika kwa ajili ya timu hiyo iliyokuwa safarini ikielekea mjini Bukoba tayari kwa mchezo huo.
Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka aliyewakilisha wabunge wengine kutoa fedha hizo amesema katika mchanganuo wa kiasi hicho, Dk Tulia ametoa Shilingi 2,000,000 huku wabunge wengine wa Mbeya wakichanga Shilingi 1,000,000.
“Tumekutana na timu kuwapa motisha kuhakikisha wanafanya vizuri kuepuka kushuka daraja kulingana na nafasi waliyopo, tumeona tuwachangie fedha kidogo kuchangia ushindi na pia tukazungumza nao kwamba kuanzia sasa tutanunua ushindi katika michezo yote zilizobaki,” amesema Kasaka.
Amesema kuwa hamasa hiyo itafanyika pia kwa viongozi wengine wa Mbeya kuanzia mechi ijayo, hiyo ni kuhakikisha timu hiyo ambayo ni kama nembo ya wananchi wa Mbeya haishuki daraja mwisho wa msimu huu.
City inashika nafasi ya 13 kwa pointi 27 baada ya mechi 26 ambapo ukiachana na Kagera Sugar, imebakiza pia kuumana na Geita Gold, Young Africans na KMC kabla ya kufungwa rasmi kwa pazia la ligi mwezi ujao.