Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na mwenzake wa viti maalum, Anatropia Theonest wamechukua hatua ya kupinga mahakamani zoezi la bomobomoa linalotarajiwa kuanza hivi karibuni katika maeneo yao, wakitaka serikali iangalie makosa yake.

Wabunge hao wakiongozwa na wakili Dk. Onesmo Kyeuke wametinga leo Mahakama Kuu Kitengo cha ardhi kupinga ubomoaji, huku serikali ikiendelea kuweka alama za ‘X’ kwenye nyumba za wakazi wa maeneo hayo.

Akizungumza jana katika mkutano na wananchi ambao nyumba zao zimewekewa alama ya ‘X’, Waitara alisema kuwa wanaenda mahakamani kupinga kwa kuwa serikali imeegemea katika upande mmoja wa mkosaji ambaye ni raia na kusahau upande wake.

“Serikali inapaswa kujihoji kabla ya kuanza mchakato huo kwa nini walikubali kupima viwanja vyao na kuwawekea mawe ya alama za umiliki wa ardhi pamoja na kupokea kodi ya majengo,” alihoji Waitara.

Alisema kuwa kitendo cha serikali kwa kushirikiana na NEMC kuingia katika maeneo ya wakazi hao na kuweka alama za ‘X’ bila kuwapa taarifa awali ni uvamizi wazi.

Mbunge huyo aliongeza kuwa wananchi wake wamepata matatizo makubwa kutokana na zoezi hilo kwa kuzingatia kuwa baadhi ya akina mama walikuwa wamechukua mikopo na kuendeleza nyumba zao huku wakilipa taratibu lakini hivi sasa nyumba hizo zinavunjwa, hivyo kwao ni tatizo kubwa.

 

Ronald Koeman Asimamia Msimamo Wake
Van Gaal: Marouane Fellaini Ni Wahapa Hapa