Taarifa kutoka ndani ya Simba SC, zinaeleza kuwa, uongozi wa timu hiyo umeweka pesa ya maana ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi dhidi ya Young Africans katika mchezo wa Kariakoo Dabi.
Simba SC ndio wenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kufanyika Jumapili (Novemba 05) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.
Chanzo kutoka Simba SC, kimeeleza kwamba, uongozi wa timu hiyo umeungana na baadhi ya mabosi ambapo wameweka kiasi kisichopungua shilingi milioni 500 ambayo ni sawa na nusu bilioni ili kuhakikisha wachezaji wanapambana kuipa timu ushindi.
“Simba wameona nafasi kubwa ya kuutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu ni kupitia mchezo dhidi ya Young Africans, kwa kuwa wakishinda basi wataiacha Young Africans Pointi sita endapo watashinda pia kiporo chao kimoja.
“Hivyo mabosi wa Simba SC wameungana pamoja na viongozi na kimepatikana kiasi kisichopungua shilingi milioni 500 ambazo watapewa wachezaji na benchi la ufundi wagawane endapo wataifunga Young Africans,” kimesema chanzo hicho.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Salim Abdallah “Try Again’, alisema: “Kuhusu bonasi za ushindi wa wachezji kuelekea mchezo wetu dhidi ya Young Africans, hatuwezi kusema hadharani ili kulinda wachezaji wetu ambao wanafamilia zao, hivyo kikubwa niwaambie kuwa malengo yetu kuelekea mchezo huo ni kwenda kumfunga mtani wetu.”