Benchi la ufundi la Young Africans limewapa mapumziko ya muda mfupi wachezaji wa klabu hiyo, baada ya kuwasili jijini Dar es salaam, jana Jumatano (Mei 26) wakitokea mkoani Shonyanga kupitia jijini Mwanza.
Young Africans iliwasili jijini humo ikiwa na uhakika wa kucheza nusu fainali ya kombe la Shirikisho ‘ASFC” baada ya kuifunga Mwadui FC mabao 2-0, Jumanne (Mei 25) katika Uwanja wa CCM Kambarage.
Kocha mkuu Nassredine Nabi amesema baada ya ushindi huo na kutokuwa na mchezo wowote hivi karibuni ameona ni bora awape mapumziko ya muda mfupi wachezaji wake.
“Nimewapumzisha wachezaji wangu baada ya kutoka katika mechi ngumu, tumeshinda na tutarejea kambini siku sio nyingi kwa ajili ya kuendelea na programu zangu.”
Hata hivyo taarifa zisizo rasmi zinaeleza kuwa, huenda kikosi cha Young Africans kikacheza mchezo wa kirafiki kwa lengo la kuiweka timu hiyo katika utayari wa michezo ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Young Africans itacheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting Juni 17, huku upande wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho itacheza dhidi ya Biashara United Mara FC mwezi ujao kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mkoani Tabora kati ya Juni 24-28.