Jumuiya ya Wafanyabiashara wa soko Kariakoo wamekubali kuendelea kufanya biashara katika soko hilo baada ya Serikali kuridhia kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakibili huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiahidi kukutana na wafanyabiashara hao Mei 17, 2023 ili kupata suluhisho la kudumu.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Waziri Mkuu kufika katika soko hilo na kuzungumza nao kufuatia mgomo ulioanza mapema Mei 15, 2023 ambapo walilalamikia masuala mbalimbali ikiwemo usumbufu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA.

Wakizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Wafanyabiashara hao wamesema, “wafanyabiashara, tumesikia maelekezo yako, lakini nilikuwa nakuomba sababu kesho kutwa tunakaa kikao, wafanyabiashara tukubali na tumuunge mkono, tufungue maduka yetu na tukimaliza kikao cha kesho kutwa tunaamini kero zetu zote zitakuwa zimekwisha”

Awali Akizungumza na Wafanyabiasha hao, Majaliwa ameiagiza TRA kusitisha matumizi ya kikosi kazi ambacho kilikuwa kinafanya kazi ya ukusanyaji wa kodi katika eneo hilo “Task force hii ndiyo inaendesha kamatakamata kila siku, Kamishna wa Mapato ya Ndani wa TRA naagiza isitishwe, kanuni zipo, sheria zipo zinatuelekeza namna ya kulipa kodi, kamatakamata hii inafukuza wafanyabiashara Kariakoo.”

Aidha, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa TRA wanaosimamia ukusanyaji wa kodi katika eneo hilo na nchini kote kutekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya namna bora ya ukusanyaji wa mapato na kuacha kutumia nguvu wanapo tekeleza majukumu yao.

“Rais Dkt. Samia ameagiza kutolewa kwa elimu ya mlipa kodi, ili walipe kwa ustaarabu lakini kama unafuata kodi na mtu amejisahau, nenda kamkumbushe kwa utaratibu, kamatakamata inachangia kuua biashara na maduka mengi yatafungwa.”

Young Africans yajizatiti Afrika Kusini
Mgogoro kati ya wanyama, Wafugaji: Simba 10 wauawa