Jeshi la Polisi Wilaya ya same Mkoni Kilimanjaro limeagizwa kuwatafuta wafugaji wanaodaiwa kuingiza mifugo katika mashamba ya watu na kuwajeruhi wakulima watatu wa kijiji cha Kisiwani-Barazani, kata ya Kisiwani, wilayani humo.
Maagizo hayo yametolewa na DC Kasilda Mgeni akiwa katika kijiji hicho kuzungumza na wananchi na kujionea athari zilizojitokeza baada ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kuwajeruhi wakulima watatu na hivyo kuagiza wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Ameagiza wafugaji wote ambao wameingia kinyemela bila kufuata taratibu za kisheria kuondoka mara moja kabla msako haujaanza na watakaobainika kukaidi agizo hilo sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.
Amewasihi wakazi wa kijiji hicho ambao wengi wao ni wakulima kuendelea kuwa watulivu wakati vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea na kazi yake, na hivyo waache kujichukulia sheria mkononi kwa kutaka kulipizia kisasi.
Licha ya hayo amewataka watendaji na viongozi wa vijiji ndani ya wilaya hiyo kusimamia sheria na kuacha tabia ya kuwapokea wafugaji wageni wanaoingia kinyemela bila kufuata taratibu za kisheria.
DC Mgeni, wafugaji wageni wanaoingia kinyemela katika wilaya hiyo mara nyingi wanaosababisha uvunjifu wa amani kwa kutoheshimu shughuli za watu wengine zinazofanyika ikiwemo kuingiza mifugo kwenye maeneo ya mashamba.