Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka wafugaji kununua ardhi na kufuga kisasa kwa kuweka miundombinu muhimu ya kuwezesha kufanikisha zoezi hilo ili kukuza uchumi wao na Taifa.
Ulega ameyabainisha hayo akiwa katika Shamba la Mifugo la Maloloi lililopo Kijiji cha Milama Kata ya Dakawa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, ili kujionea namna mtanzania mwenye asili ya kimasai alivyobadilisha ufugaji wa kiasili na kufuga kisasa.
Amesema, wafugaji wanatakiwa kubadilika na kuondokana na migogoro ya ardhi zilizosababishwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, hivyo waache ufugaji wa kuhamahama na badala yake wanunue ardhi na kuwa na mifugo wanayoweza kuihudumia.
Ameongeza kuwa, “Ni muhimu wanunue ardhi na waimiliki kwa mujibu wa sheria, inasajiliwa kwa ajili ya ufugaji anaweka na miundombinu kama majosho na kisima kikubwa cha maji kwa ajili ya uhakika wa kupata maji, itasaidia kuinua sekta.”
Ulega pia, amewataka wataalam wa sekta ya mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kufika katika Shamba hilo la Maloloi kumsadia kulisajili na kulitambua kuwa ranchi ya sekta binafsi kwa wafugaji wa asili waliobadilika.
Kwa upande wake mmiliki wa Shamba hilo la Mifugo, Maloloi Kibangashi amesema aliamua kuacha kufuga kwa njia ya asili kwa kuuza mifugo hiyo na kununua ng’ombe wa kisasa wakiwemo wa nyama na maziwa ili kuepuka kuhamahama.
Ametoa rai kwa wafugaji wengine kubadilika kwa kufuga kisasa ule wa asili umekuwa ukisababisha migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima, hivyo kuuza mifugo waliyonayo na kubakiza michache ambayo wanaweza kumudu kuwa nayo na kufuga kisasa.
Naye, Afisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Bi. Natujwa Melau amesema wilaya hiyo ina wafugaji wengi, ambao wamekuwa wakihamasishwa ufugaji wa kisasa ili kuepuka migogoro kwa kupitisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha wafugaji wanabadilika na kufuga kisasa kwa kuwa na mifugo bora inayotoa nyama na maziwa na kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hasa wakulima.