Takribani wafungwa 900 wameripotiwa kutoroka kutoka katika gereza moja la eneo lililo Kaskazini mwa mji wa Beni, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), baada ya watu wenye silaha kushambulia gereza hilo.
Gavana wa jimbo la Kivu Kaskazini, Julien Paluku amesema kufuatia shambulio hilo watu 11 waliuawa.
Ingawa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo, chanzo kimoja kimeliambia shirika la habari la Uingereza (BBC) kuwa huenda wanajeshi wa kundi la Mai-Mai ndio waliotekeleza shambulizi hilo.
Hili sio tukio la kwanza dhidi ya magereza nchini humo. Mwezi uliopita, mamia ya wafungwa waliripotiwa kutoroka katika jela moja kubwa mjini Kinshasa, baada ya mtu mmoja mwenye silaha kufanya mashambulizi usiku wa manane.
DRC imekuwa ikikabiliwa na vitendo vya mashambulizi ya aina hiyo kutokana na kuwepo makundi mbalimbali yanayoendesha mapigano dhidi ya Serikali, kutaka kuwatoa magerezani wafuasi wao wanaoshikiliwa.