Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameagiza sheria za madini zipitiwe upya ili kuepusha wizi unaofanywa na makampuni ya madini nchini.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo baada ya kupokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa usafirishaji wa mchanga wa madini, iliyofanywa na Kamati maalum ikiongozwa na Profesa Nehemia Osoro.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyoanisha mapungufu mbalimbali imeeleza kuwa Serikali imepoteza zaidi ya shilingi trilioni 108 uliotokana na ukwepaji wa kodi mbalimbali uliofanywa na makampuni ya madini tangu mwaka 1998.

Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi kuunda timu ya wanasheria waaminifu ambao watapitia mikataba hiyo hatua kwa hatua ili kuhakikisha hakuna sheria kandamizi kwa maslahi ya taifa.

Alishangaa uwepo wa wasomi nchini katika sekta mbalimbali, lakini nchi imeendelea kuibiwa katika sekta ya madini kwa kiwango cha kushangaza.

“Pale BOT kuna Phd 17, na haya ndio matokeo. Wanasheria wako wengi wamefundishwa na Profesa Kabudi, sifahamu alikuwa anawafundisha nini, wakiingia kwenye mikataba kama hii sheria yote inapotea. Wanasaini chochote wanachoambiwa. Na wakati mwingine draft (rasimu) ya mikataba inatoka imeandaliwa kule, wao wanakuja kupitisha tu,” alisema Rais Magufuli.

“This is the country… tumelogwa na nani? Basi kama tumelogwa mtuombee ninyi mapadri, wachungaji na mashehe. Kama ni mapepo basi yakaondoke,” aliongeza Rais Magufuli.

Aidha, amevitaka vyombo vya habari kuwahoji na kuwachukulia hatua wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo ikiwa ni pamoja na mawaziri wastaafu waliotajwa, isipokuwa marehemu Abdallah Kigoda.

Rais Magufuli aliongeza kuwa iwapo kampuni ya madini ya ACACIA itakubali makosa yake na kutubu, Serikali itakuwa tayari kufanya majadiliano.

Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ameahidi kuunda tume maalum kuchunguza masuala ya madini ya almasi.

Video: Kamati yabaini ACACIA haijasajiliwa nchini, Serikali yapoteza sh. Trilioni 55
Wafungwa zaidi ya 900 watoroka gerezani, gereza lashambuliwa