Aliyekuwa mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (Chadema) jana aliibuka katika kanisa la Ufufuo na Uzima linaoongozwa na askofu, Josephat Gwajima, ikiwa ni miaka miwili ya ukimya wake mbele ya hadhara.

Nyerere ambaye alijitanabaisha kuwa rafiki wa askofu huyo, aliwasalimu waumini wa kanisa hilo.

“Mimi naitwa Nyerere… lakini ni Mkatoliki niliyebatizwa nikapewa jina la Vincent. Baba yangu anaitwa Josephat [Kiboko Nyerere], na wanaomjua ni jasiri kama alivyo Askofu Gwajima.

Nilimuomba Askofu nije kushiriki nanyi, mimi ndiye niliyemuomba. Ni mara yangu ya kwanza kuja Ufufuo na Uzima lakini naomba isiwe mara ya mwisho,” alisema Nyerere.

Aliungana na mahubiri ya Gwajima akiwataka watanzania kuondoa hofu katika kufanya maamuzi yao ili waweze kuwa na amani mioyoni mwao.

Aidha, alieleza kupinga gharama za kukimbiza Mwenge wa uhuru akidai kuwa kama taifa inahitajika tafakari ya umuhimu wa mwenge huo katika nyakati hizi.

Hii ni mara ya kwanza kwa mbunge huyo wa zamani wa Musoma kuonekana akizungumza hadharani baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 na aliyekuwa mshindani wake mkuu, Vedastus Mathayo (CCM).

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara ambaye pia alihudhuria ibada hiyo, alipewa nafasi ya kuwasalimia waumini. Alitumia nafasi hiyo kueleza jinsi ambavyo hakuridhishwa na Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2017/2018 iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Wafungwa zaidi ya 900 watoroka gerezani, gereza lashambuliwa
Mtoto wa Gaddafi akwepa kifo Libya, asakwa na ICC