Saif al Islam Gaddafi, mtoto wa aliyekuwa rais wa Libya, Muamar Gadaffi ameachiwa huru kutoka gerezani alikokuwa akishikiliwa akisubiri hukumu ya kifo.

Saif ambaye ni mtoto wa pili wa marehemu Gaddafi, alikuwa akitajwa kuwa ndiye anayeweza kuwa mrithi wa baba yake akiwa na uwezo mkubwa wa kuhamasisha na kuongoza jeshi la nchi hiyo wakati wa vita iliyomaliza utawala wa baba yake.

Baada ya vita hiyo ya mwaka 2011, alikamatwa jangwani akijaribu kutoroka kueleka nchi ya Niger, na alishtakiwa kwa makosa ya uchochezi na mauaji ya watu waliokuwa wakipinga utawala wa baba yake.

Mwaka 2015, alihukumiwa kifo kwa kupigwa risasi na vikosi vya jeshi, hukumu iliyotolewa kwa wafuasi 30 wa karibu wa Gaddafi.

Mwanasheria wake, Khaled al-Zaidi amethibitisha kuwa mteja wake aliachiwa huru ijumaa iliyopita, lakini hakuweka wazi alielekea mji gani kwa sababu za kiusalama.

Imeelezwa kuwa Seif ameachiwa kufuatia makubaliano ya Serikali mbili zinazopambana nchini Libya, moja ya Tripoli iliyosimikwa baada ya kuondolewa kwa Gaddafi, na nyingine ambayo ni tiifu kwa marehemu Gaddafi.

Kuachiwa kwa Saif ambaye aliwahi kutunikiwa shahada ya uzamivu na chuo kikuu cha London mwaka 2008, kumeongeza hofu kuwa huenda kukachangia zaidi kuvitia moyo vikosi vinavyomuunga mkono Gaddafi, vinavyoendelea kupambana na serikali ya Tripoli, iliyosimikwa baada ya kuuawa kwa Gaddafi.

Hata hivyo, Saif anatafutwa pia na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai kwa makosa ya kivita na mauaji ya halaiki.

Nyerere aibukia kwa Gwajima
?BREAKING NEWS: Rais Magufuli Akipokea Ripoti ya Pili ya Makinikia