Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Wanafunzi 1,206,995 kati ya 1,397,370 waliohitimu darasa la saba mwaka huu wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo Januari, mwakani.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Januari 30, mwakani.
Amesema, “Wanafunzi 1,206,995 sawa na asilimia 86.4 ya wanafunzi 1,397,370 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2023 wanatarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari Januari, 2024.”
Majaliwa ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kukamilisha maandalizi muhimu ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2024 ikiwemo ujenzi wa miundombinu. “Nitumie fursa hii kuwakumbusha Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wote nchini wahakikishe kuwa ujenzi wa miundombinu yote katika shule za sekondari unakamilika kabla ya tarehe 30 Novemba, 2023.”
Amesema Serikali itawachukulia hatua wote watakaoshindwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika shule za sekondari. “Wakuu wa Mikoa fanyeni ufuatiliaji, Serikali imeshapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi katika Halmashauri zote nchini hivyo hakuna sababu wala visingizio vya kutokamilisha ujenzi kwa wakati,” amesisitiza.