Waziri wa Usalama wa Ndani nchini Kenya, Prof. Kithure Kindiki amesema shajara ya kazi yake inapangwa na wahuni na wahalifu, akiwataja kama watu ambao hawana makao chini ya utawala wa Serikali ya Kenya Kwanza.
Prof. Kindiki ameyasema Jumapili, Julai 16, 2023 huku akibainisha kuwa binafsi hana ratiba maalum kwani wahalifu ndio huamua atakapoenda na hatua zitakazochukuliwa dhidi yao kwani ni watu wanaohatarisha amani ya Taifa.
“Shajara yangu inapangwa na watu wengine, na si watu wazuri. Inapangwa na magaidi wa Al Shabaab, wezi wa mifugo wahuni na wahalifu hao ndio wana ratiba yangu kamili na wao ndio huamua leo nielekee wapi,” amebainisha Prof. Kindiki.
Aidha, Waziri huyo pia ameliorodhesha kundi la Al – Shabaab, wezi wa mifugo wa Bonde la Ufa, wahubiri matapeli, wauzaji wa pombe haramu na dawa za kulevya, maandamano ya muungano wa Azimio la Umoja na uhalifu mwingine kama kero ambazo zinamnyima usingizi.