Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan anawasihi waislamu na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuonesha upendo, umoja na mshikamano hata baada ya kumalizika kwa masiku kumi bora katika mwaka yanayopatikana kwenye mwezi wa Dhul-Hijja.

Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 10, 2022) kwenye Baraza la Eid El Adha, lililofanyika katika Msikiti wa Mfalme Muhammad wa Sita wa Morocco uliopo Kinondoni, Dar Es Salaam. Ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi umuhimu wa kudumisha amani.

Waziri Mkuu pia ametumia fursa hiyo naye kuwasihi waislam kuendelee kudumisha amani, upendo, umoja, mshikamano, kuhurumiana, utulivu sambamba na kujiepusha na vitendo vinavyoashiria vurugu, uonevu na uvunjifu wa amani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitoka kuswali Swala ya Eid al- Adha kwenye Msikiti Maarufu kwa jina la ‘Msikiti wa Mwinyi’ Mikocheni B Jijini Dar es Salaam hii leo Julai 10, 2022.

“Moja ya jambo adhimu katika Eid El Adha ni kuchinja na jambo hilo limethibitika katika Qur’an Tukufu pale Allah Ta’ala aliposema katika surah ya 108 ayah ya pili kwamba basi swali kwa ajili ya Mola wako na chinja kwa ajili yake,” amebainisha Majaliwa.

Ameongeza kuwa, “Hivyo basi, nami nahimiza kwamba tutumie fursa hiyo ya kuchinja kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fadhila mbalimbali alizotujalia pamoja na kuwahurumia na kuwaonesha upendo wenzetu wakiwemo maskini.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wote wa dini nchini na vyombo vya Habari kwa kuendelea kuelimisha na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajia kufanyika nchini kote Agosti 23, 2022.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi pia amejumuika na Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Eid El Hajj Msikiti wa Jitimai, Kidoti Mkoa wa Kaskazini leo tarehe: 10 Julai, 2022.

Aidha, pia amempongeza Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally pamoja na Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA), kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuiunga mkono Serikali katika utoaji na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii.

Kwa upande wake, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally amewaagiza Masheikh wa mikoa na wilaya kuendelee kuwahimisha waislamu kujitokeza kuhesabiwa kwakuwa sensa ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwa amejumuika katika Baraza la Eid El Adha, lililofanyika katika Msikiti wa Mfalme Muhammad wa Sita wa Morocco uliopo Kinondoni, Dar Es Salaam hii leo Julai 10, 2022.

Rais, Waziri Mkuu wathibitisha kuachia ngazi
Watu 14 wauawa, wauaji wafyatua risasi hovyo katikati ya Mji