Baadhi ya wafanyabiashara wa mazao jamii ya matunda, wameiomba Serikali kujitokeza hadharani kuzungumza iwapo inatambua kiwango cha nguvu kazi kinachopotea, juu ya uzalishaji mwingi wa mazao usio na tija kwa kukosa soko la uhakika hali inayopelekea mazao yao mengi kuoza na kutupwa.
Wakizungumza na Dar24 kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao wa mazao jamii ya matunda wamesema, wamekuwa wakipambana na wakati mgumu kwani sehemu kubwa ya mazao yao imekuwa ikiharibika kutokana na kukosa wateja wa uhakika na hivyo kupelekea kuingia hasara na kujutia muda uliopotea.
Joseph Mwalikifi, mmoja wa wafanyabiashara hao amesema, “Angalia hizi nyanya hapa zinaoza tu hakuna soko la uhakika maana nazivuna shambani naleta hapa barabarani lakini zitakaa mpaka zinaharibika na ukumbuke nilitumia fedha na Dawa wakati wa maandalizi yote ya kilimo Serikali ituangalie.”
Naye, Mfanyabiashara Mohamed Mohamed amesema ipo haja ya kuangalia soko la uhakika ikiwemo kuanzisha viwanda vya usindikaji kwa ajili ya kununua matunda moja kwa moja kutoka shambani na machache kwa mtindo wa rejareja tofauti na ilivyo sasa kwani wengi wao hawaoni faida yake.
“Hapa kuna nyanya, machungwa, ndizi, mapapai, matikiti, lakini utokaji wake ni wa kusuasua kama Serikali ingeweza kutusaidia kutafuta soko la uhakika tungekuwa tumejikwamua lakini tunaishia kupambana na wachuuzi na wao tunawauzia kwa bei ya chini sana ukisema ukatae utakula wapi,” amebainisha Mohamed.
Hata hivyo, wamesema wana imani kuwa Serikali inalifahamu na kwamba huenda Wizara husika inalifanyia kazi na kwamba wanamtaka Waziri mwenye dhamana kutokaa kimya na badala yake ajitokeze hadharani kuelezea mikakati husika juu ya uharibifu unaotokea na hatua zinazotarajiwa kuchukuliwa.