Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seif kusitishia mikataba ya wakandarasi wababaishaji na walioonesha uwezo mdogo kwenye utekelezaji wa miradi ya barabara.
Shaka ameyasema hayo wakati akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi wa Tabora Kaskazini, baada ya kukagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari Gilimba iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora na kusema wakandarasi hao pia wanatakiwa kutopewa kazi na TARURA nchini.
Amesema, “Inasikitisha TARURA mnakiri hapa kuwa mmepokea fedha shilingi milioni 499 na mkasaini mkataba na mkandarasi mwezi Juni 2021 ambao alipaswa kuikamilisha kazi ndani ya miezi sita, leo ni mwezi Agosti, 2022 miezi 14 tangu mpokee fedha na kumpata mkandarasi bila kazi kukamilika.”
“Wawakilishi wa wananchi wamelalamika mkandarasi hana uwezo na ninyi TARURA mmekiri hilo ila mnafikiria kuvunja mkataba wake mpaka sasa, ushauri wangu vunjeni mkataba na mkandarasi huyo na wengine wote ambao hawafanyi vizuri ili wapewe kazi wakandarasi wenye uwezo wa kufanya kazi kwa viwango na kasi inayotakiwa,” amesisitiza Shaka.
Agizo la Shaka, limetolewa kufuatia Wananchi wa kata ya Igulungu, Jimbo la Tabora Kaskazini, kulalamikia ubovu wa barabara yao ambayo ina mkandarasi anayefanya kazi kwa kiwango cha chini na kwa kusuasua licha ya kulipwa sehemu ya fedha za utekelezaji wa mradi huo
Katika kuhakikisha inapeleka huduma kwa wananchi na kuboresha mawasiliano ya miundombinu ya barabara, hasa maeneo ya vijijini, Serikali imeiongezea fedha TARURA kutoka shilingi 276 bilioni, hadi shilingi 750 bilioni katika mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo Jimbo la Tabora Kaskazini lilipata shilingi bilioni 1.5.