Waziri wa Nishati, January Makamba amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy kutosaini mikataba miwili na Kampuni ya ETDCo kutokana na utendaji usioridhisha.
Makamba ameyasema hayo Desemba 19, 2022 na kuongeza kuwa Kampuni hiyo imeonyesha udhaifu mkubwa kwenye utekelezaji wa miradi kadhaa ya kupeleka nishati vijijini ukiwemo wa Mkoani Mbeya ambapo imefanya kazi kwa asilimi 28 mpaka sasa.
“ETDCo leo hakuna kusaini mkataba wa Mradi wa PERI Urban III, nendeni kwanza mkakamilishe kazi mkoani Mbeya na Katavi, nimeona kwenye Mradi wa PERI Urban mmeshinda zabuni ya mkoa wa Kigoma na Geita na kazi zote hizo zina thamani ya shilingi bilioni 18,” amesema Waziri Makamba.
Aidha, ameongeza kuwa, “Hii si sawa na mmeshindwa kutekeleza miradi kwa wakati, mfano mkoani Katavi kwa kazi ile mlitakiwa hadi sasa walau mngekuwa mmefika asilimia 81 ya utekelezaji lakini bado utekelezaji upo chini.”
Hata hivyo, Waziri Makamba amesema kuanzia sasa Wakandarasi wa ndani watapimwa kwa utendaji (Performance) na si vinginevyo na kuongeza kuwa Wakandarasi ambao utendaji wao ni wa mashaka, wasahau kupata Miradi ya REA.
Wakati huo huo, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imesaini Mkataba wa PERI Ubani Awamu ya Tatu. Mradi huo una lengo la kupeleka umeme katika maeneo ya pembezoni mwa miji. Mikoa ambayo imelengwa ni pamoja na Geita, Mtwara, Mbeya, Tabora, Tanga Singida na Kigoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy tayari amesaini mikataba kwa niaba ya Serikali jijini Dar es Salaam na Watendaji wa Kampuni nne ambazo ni Central Electricals International Ltd, DERM Electrics (T) Ltd, OK Electrical & Electronics Services Ltd na DIEYNEM Co Ltd.