Kenya imeongezwa kwenye orodha ya nchi zilizowekewa vikwazo vya kusafiri na Uingereza huku kukiwa na wasiwasi juu ya kuenea kwa aina mpya ya virusi vya corona.
Kuanzia tarehe 9 Aprili, wageni wa kimataifa ambao wamesafiri kutoka au kupitia Kenya, pamoja na Ufilipino, Pakistan, na Bangladesh katika siku 10 zilizopita hawataruhusiwa kuingia Uingereza.
Hata hivyo wamiliki wa pasi za kusafiria za Uingereza au Ireland, au watu walio na haki za makazi ya Uingereza hawaguswi na marufuku hii , lakini lazima wawekwe karantini kwa siku 10, katika hoteli iliyoidhinishwa na serikali, kwa gharama zao.
Watu hao pia watalazimika kuchukua vipimo viwili vya virusi vya corona – lakini matokeo hasi ya vipimo (negative) hayamaanishi kuwa wanaweza kufupisha muda wao katika karantini.
Hakuna marufuku ya moja kwa moja ya kusafiri kutoka nchi hizo itakayowekwa lakini abiria wanashauriwa kuangalia mipango yao ya kusafiri kabla ya kuondoka kwenda Uingereza.
Ubalozi wa Uingereza umeiarifu Kenya kuhusu mipango ya kuiongeza Kenya katika orodha ya karantini inayohusisha ugonjwa wa Covid-19.
Taarifa kutoka ubalozi ilisema uamuzi huo mgumu ulichukuliwa na Mawaziri wa Uingereza Machi 31 kufuatia tathimini ya ushahidi wa hivi karibuni wa kisayansi unaohusu hatari ya usambaaji wa Covid-19 katika jamii.
Orodha kamili ya nchi zilizo chini ya marufuku ya kusafiri sasa ni pamoja na Angola, Argentina, Bangladesh Bolivia, Botswana, Brazil, Burundi, Cape Verde, Chile, Colombia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ecuador, Eswatini, Ethiopia, Guiana ya Ufaransa, Guyana, Kenya, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Namibia, Oman, Pakistan Panama, Paraguay, Peru, Ufilipino, Qatar, Rwanda, Ushelisheli, Somalia, Afrika Kusini, Suriname, Tanzania, Falme za Kiarabu (UAE), Uruguay, Venezuela, Zambia na Zimbabwe.
Wanadiplomasia nchini Uingereza, maafisa, watumishi au wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, na wale walio na kinga za kidiplomasia, na familia zao au wategemezi, hata hivyo, hawahitaji kujaza fomu za abiria na hawalazimiki kupima virusi vya corona.
Pia hawatalazimika kukaa karantini katika hoteli iliyoidhinishwa na serikali lakini wataombwa kujitenga katika eneo watakaloishi nchini Uingereza kwa siku 10 baada ya kuwasili.
Ubalozi wa Uingereza umesema hizi ni hatua za muda mfupi na zitakuwa zikipitiwa.
Vizuizi vya kusafiri vitabaki tu wakati kiwango cha hatari kinatathminiwa ili kuhalalisha hatua hizi.
Nchi kadhaa pamoja na Ureno na Mauritius zimeondolewa kwenye orodha ya karantini kwa sababu ya hatua zilizoletwa kupunguza hatari inayosababishwa na aina tofauti za virusi vya corona, pamoja na kuongezeka kwa ufuatiliaji kupunguza hatari inayosababishwa na virusi.