Kutokana na jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa Pembejeo zikiwemo mbolea, hadi Oktoba 31, 2023 Wakulima zaidi ya milioni 3.6 walikuwa wamesajiliwa na kupata namba za utambulisho za kununua mbolea ya ruzuku.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge jijini Dodoma ambapo Bunge hilo limeahirishwa hadi Januari 30, mwakani.
“Wakuu wa Wilaya wawahamasishe Wakulima kujisajili na kutoa taarifa sahihi kuhusu mazao wanayolima na ukubwa wa mashamba yao kwenye madaftari ya wakulima ambayo yamesambazwa kwa watendaji wa Vijiji na Mitaa ili taarifa zao ziweze kuingizwa kwenye mfumo na wapatiwe namba za kununulia mbolea ya ruzuku,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, ameitaka Wizara ya Kilimo ihakikishe mbolea inapatikana kwa wakati na ishirikiane na Wakuu wa Wilaya kusimamia kwa karibu usambazaji wa mbolea kwa wakulima. “Hatua hii iende sambamba na kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa usambazaji wa pembejeo hiyo muhimu,” amesisitiza.
Hata hivyo, amezitaka kampuni na taasisi zinazozalisha mbegu bora ziongeze kiwango cha uzalishaji na kuweka utaratibu mahsusi wa kufikisha mbegu hizo kwa wakulima katika maeneo yao ya uzalishaji.