Maelfu ya walimu wa shule za msingi katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria wameshindwa kufikisha alama za ufaulu walipofanya mtihani ulioandaliwa kwa ajili ya wanafunzi wenye umri kati ya miaka sita na saba.
Gavana wa jimbo hilo, Nasir El-Rufai akizungumza katika mkutano na wawakilishi wa Benki ya Dunia, alisema kuwa walimu 21,780 waliopewa mtihani huo wa wanafunzi walishindwa kupata asilimia 75 za ufaulu.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, walimu hao wameondolewa kwenye mfumo wa ajira ya walimu mara moja na kwamba Serikali inaaandaa walimu wapya 25,000 kwa ajili ya kuziba pengo hilo.
“Mpango wa ajira kwa walimu hapo awali ulikubwa wa kisiasa. Sasa tumedhamiria kubadili hali hiyo kwa kuajili walimu vijana wenye sifa za kuwa walimu wa shule za msingi ili turudishe heshima na hadhi ya elimu katika jimbo letu,” Gazeti la Nigeria la Daily Trust linamkariri.
El-Rufai aliongeza kuwa tatizo la uhaba wa walimu katika nchi hiyo pia litashughulikiwa ipasavyo.
Alisema maeneo mengi yana wastani wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 100 wakati maeneo mengine yana wastani wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi tisa.