Mamia ya Waandishi wa habari na wanaharakati wa kisiasa, wameandamana katika mji mkuu wa Senegal, Dakar kutaka kuachiliwa huru kwa mwandishi wa Habari na mkosoaji wa Serikali, Pape Ale Niang aliyewekwa kizuizini Novemba 9, 2022.
Niang, ambaye anaendesha tovuti ya Habari za mtandaoni ya Dakar Matin, amekuwa akiikosoa serikali ya Rais Macky Sall na alikamatwa Novemba 6, 2022 akishtakiwa kwa makosa ya uchochezi na kuwekwa chini ya amri ya kizuizini siku tatu baadaye.
Moja ya mashitaka yanayomkabili ni pamoja na kutuhumiwa kutangaza jumbe za siri kuhusu mipango ya usalama kuhusiana na mahojiano ya Novemba 3 ya mwanasiasa wa upinzani Ousmane Sonko kuhusu madai ya ubakaji na kueneza habari za uongo.
Makamu wa rais wa kongamano la wanahabari vijana wa Senegal, Migui Marame Ndiaye, amesema wamekusanyika ili kushinikiza kuachiliwa kwake, wakidai nafasi ya Pape Alé Niang si gerezani bali ni kwenye chumba cha habari.
Kuzuiliwa kwake kumezua wimbi la ukosoaji kutoka kwa waandishi wa habari na mashirika ya kiraia dhidi ya rais wa Senegal ambapo Mwandishi wa habari na mwanaharakati, Nina Penda Faye, alisema bado kuna Wanasiasa, Wsenegal na waandishi wa habari ambao wamefungwa kimakosa.
Amesema, “Tunataka hili likome na tunaomba Jimbo la Senegal, tunaomba hasa viongozi wetu kuwaachilia mateka wote akiwemo Pape Alé Niang ambaye alizuiliwa kwa makosa ya vyombo vya habari.”
Senegal, imeorodheshwa kuwa ni ya 73 kati ya nchi 180 kwenye Fahirisi ya Dunia iliyoandaliwa na Waandishi Wasio na Mipaka ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ya 2022.