Serikali imesema, itaendelea kutatua changamoto za migogoro ya mipaka kati ya Hifadhi na Wananchi, ili kuleta ufahamu wa maeneo ya Vijiji na kuheshimu mipaka ya Hifadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma hii leo Juni 28, 2022 wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi, Aida Joseph Khenani aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupitia mipaka ya Hifadhi na Makazi ya Wananchi wa Wilaya ya Nkasi.
Amesema Serikali imeweka alama 111 kati ya 322 zinazohitajika katika Pori la Akiba Lwafi Wilayani Nkasi, ili kuainisha mipaka ya hifadhi hiyo na kwamba wanaendelea na jitihada za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutambua mipaka ya Hifadhi.
“Jumla ya vigingi 111 vimewekwa kati ya vigingi 322 vinazohitajika katika Pori la Akiba la Lwafi Wilayani Nkasi, ili kuainisha mipaka ya hifadhi hiyo na Serikali itaendelea na jitihada za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutambua na kuheshimu mipaka ya Hifadhi,” amesema.
Kuhusu migogoro ya mipaka kati ya Vijiji vya Vilima Vitatu, Mwada na Ngolee na Hifadhi ya Tarangire Wilayani Babati, Waziri Masanja amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itatuma wataalam kwenda kufafanua au kutafsiri mipaka ili wananchi wajue maeneo ya vijiji.