Mwanamume mmoja na mke wake wa pili wahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kusababisha madhara mabaya mwili kwa mtoto wao wa kuzaa.
Hawa ni Joseph Ireri Njeru mwenye umri wa miaka 42, na Bi. Bancy Wanja Nyaga 30, wanaotoka kijiji cha Njakairi kaunti ya Embu huko nchini Kenya.
Wawili hao wanasemekana kumtesa na kumjeruhi vibaya mtoto wao mwenye umri wamiaka 9 kwa kumuadhibu kwa namna ya isiyo ya kawaida kwa kosa la kwenda kumtembelea bibi yake kinyume cha matakwa ya wazazi wake.
Inaelezewa Julai 2, 2021, wazazi hao walimfunga mtoto huyo mwenye umri wa miaka 9 kwenye kiti cha sofa, na kumchapa viboko mara kwa mara kwa kutumia kamba ngumu ilikuwa ikitumika kumfunga Mbwa. Na baada ya kufanya kitendo hicho, walimwagia maji ya baridi akiwa kwenye kiti hicho na kumuacha hapo kwa muda wa siku mbili mfululizo.
Ndugu wa mtoto huyo baadaye walimkomboa kutoka kwenye kiti hicho, kitendo kilichowaingiza matatani baada ya wazazi wao kubaini kitendo cha wao kumfungulia mdogo wao, hivyo nao wakaadhibiwa vikali kwa kosa la kumuokoa mtoto huyo.
Baadaye mjomba wa watoto hao aliingilia kati na kuwasilisha malalamiko juu ya matukio hayo katika kituo cha polisi kilicho karibu kitendo kilichopelekea wawili wanandoa hao kutiwa mbaroni.
Hakimu Juliana Ndengeri aliwahukumu wawili hao kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja, akisema washukiwa “hawastahili kuwa karibu na watoto”. Akitoa uamuzi huo, Hakimu Ndengeri alidokeza kuwa kwa muda ambao amefanya kazi katika idara ya mahakama hajawahi kukutana na tatizo baya lenye taswira ya kutisha lenye kuwahusisha wazazi wenye kuwadhuru watoto wao wenyewe.
Hakimu alibainisha kuwa hata baada ya kumtesa mtoto huyo, wanandoa hao hawakujishughulisha kwa namna yeyote hata kumpeleka hospitali badala yake walimficha ndani wakiamini atapata nafuu.
Kutokana na kitendo hicho Mke wa kwanza (Bi mkubwa) wa mwanamume huyo, tangu kutokea kwa tukio hilo ameihama nyumba yao.