Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Naibu Kamishna wa Polisi, DCP. Maria Nzuki amewataka Wanaume wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara wametakiwa kufunguka na kutumia Dawati la Jinsia na Watoto kutoa taarifa pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kupigwa na wake zao.
DCP Nzuki, ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Ofisi za Dawati la Jinsia na Watoto zilizojengwa kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu na Afya ya uzazi (UNFPA), kwa kushirikiana na Shirika la Utu wa Mtoto (CDF).
Amesema, “Wanaume wengi wamekuwa wakiona aibu kuripoti matukio ya kufanyia ukatili na wake zao katika Dawati jambo ambalo limekuwa likiendeleza vitendo hivyo katika jamii, hivyo ili kukomesha tabia hiyo wanapaswa kutoona aibu.”
Aidha, Nzuki ameongeza kuwa, mpaka sasa kuna madawati 420 ambayo yanaendelea kutoa huduma nchini, na kwa Mkoa wa Manyara yapo matatu ambayo yamejengwa katika Wilaya za Simanjiro, Kiteto na Mbulu na kwa kushirikiana na wadau wataendelea kuboresha ili kukidhi vigezo vilivyowekwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Sezaria Makota alisema kufunguliwa kwa dawati hilo ni ishara tosha kuwa vitendo vya ukatili vinakwenda kupungua katika Wilaya hiyo hususani ukatili kwa watoto wadogo na kwamba baadhi ya Wakazi wa mbulu wamekuwa wakiwaachia babu na bibi katika malezi ya Watoto jambo ambalo linapaswa kukemewa.
Naye, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Manyara, Yustina Rahhi alisema dawati hilo ni mkombozi katika eneo la Mbulu na mkoa wa Manyara kwa kuwa ukatili upo na takwimu siyo nzuri hivyo kila mmoja anapaswa kuchukua hatua katika kukomesha vitendo hivyo.