Wanaume nchini wametakiwa kuwa na utamaduni wa kujichunguza matiti ili kubaini viashiria vya saratani ili wasichelewe kuanza matibabu endapo wakibainika na ugonjwa huo.
Wito huo umetolewa na daktari bingwa wa Saratani, Sikudhani Muya wakati wa uchunguzi wa saratani ya matiti na utoaji elimu juu ya ugonjwa huo uliofanyika jana katika hospitali ya Mloganzila.
Hayo yamejiri ikiwa ni muendelezo wa matukio ya kuadhimisha mwezi wa utoaji elimu ya ugonjwa wa Saratani.
Miongoni mwa walioshiriki ni naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndungulile aliyesema Serikali imeelekeza nguvu katika kupambana na saratani ya matiti kwa wanawake ambao ndio waathirika wakubwa halikadharika wanaume wanaojihisi viashiria vya ugonjwa huo kufika kwenye vituo vya afya.
” Saratani ya matiti kwa wanaume ni aghalabu, inaweza kutokea ukapata mgonjwa mmoja kwa miaka 10 lakini wanawake ni tatizo linaliwasumbua zaidi” alisema Ndungulile.
Dkt. Muya alikazia, licha ya wanawake kuwa waathirika wakubwa wa saratani ya matiti wapo pia wanaume wanaopata ugonjwa huo, lakini huchelewa kujigundua kutokana na maumbile yao.
Na jambo hilo linawafanya wafike hospitalini wakiwa katika hatua mbaya kutokana na kuchelewa kupata matibabu.
Alitilia mkazo kuwa, hali ya saratani kwa wanawake imeendelea kuwa tishio kwani idadi kubwa inazidi kuongezeka na ugonjwa huo unachukua maisha yao.