Mtu na mpenzi wake (Mohammed Namkunga naAsma Rajab) wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kughushi cheti cha malipo ya korosho wilayani Newala mkoani Mtwara.
Mkuu wa wilaya hiyo, Aziza Mangosongo amesema kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa katika Kata ya Makonga baada ya kupatikana kwa taarifa kuhusu udanganyifu uliopo kwenye chama cha msingi (Amcos) cha Makonga.
Amesema wananchi walitoa taarifa baada ya kuelezwa kwamba wakiona mtu analeta korosho kinyume cha sheria kwenye chama wazijulishe mamlaka husika.
“Siku ya tukio, Namkunga alikwenda na viroba viwili vya korosho. Baada ya kufanikiwa kuviingiza, Asma aliandika kwenye cheti kuwa Namkunga amepeleka kilo 200 na kwa bei ya Sh3,300 angepata zaidi ya Sh600,000 kinyume cha sheria,” alisema Mangosongo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Geldius Byakanywa amesema kabla ya malipo, uongozi unajiridhisha wakulima wanaostahili.
Amesema chama hicho kilikuwa na lengo la kukusanya tani 400 lakini mpaka sasa kimepata tani 200.