Katika kuhakikisha jamii inakuwa na uwezo wa kutambua umuhimu wa kudai upatikanaji wa haki zao za msingi, kamati za wananchi kutoka shehia za Wilaya za Micheweni, Wete, Mkoani na Chake Chake Pemba zimeshauriwa kuendelea kuwashirikisha wananchi kujadili changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi kwa njia na wakati sahihi bila kusababisha madhara.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Tathmini na ufuatiliaji wa TAMWA Zanzibar, Mohamed Khatib
wakati wa mkutano na kamati za wananchi shehia za wilaya kisiwani Pemba, uliolenga kuzijengea uwezo kamati hizo kufuatilia kero za haki za wanawake ambazo ziliibuliwa na wahamasishaji jamii kwenye maeneo yao.
Alisema, “Ni lazima kamati hizi zikutane na wananchi ili wao wenyewe waseme wana changamoto gani kuliko kuwasemea, hii itasaidia kuwa na uthibitisho na ushahidi wa kutosha juu ya changamoto yoyote inayotafutiwa ufumbuzi.”
Awali, Mkurugenzi wa mradi PEGAO, Hafid Abdi, alisema jamii inapaswa kutambua wajibu wake ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili huku Mratibu TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa, akisema “haki haisubiriwi, haki inatafutwa, hivyo ni lazima wananchi wawe na uelewa wa kutosha juu ya zipi ni haki zao na namna gani wanapaswa kudai haki zao kwa njia iliyo sahihi.”