Watafiti wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), wamebaini fursa mbalimbali zilizoko kwenye majitaka ya vyooni na kinyesi cha bindamu, ikiwemo fursa ya gesi ya majumbani, mbolea na maji ya kumwagilia mashambani ambayo yamesafishwa kutokana na majitaka kutoka vyooni na kinyesi.
Hayo yamebainishwa na watafiti hao kwenye kituo cha utafiti chuoni hapo walipokuwa wakielezea namna wanavyozalisha mbolea na gesi katika kituo cha cha utafiti cha Sanitation Biotechnologies Research Center chuoni hapo.
Akizungumza na Dar24Media mmoja wa watafiti hao, Edward Ruhinda ambaye ni Mtafiti wa Shahada ya Uzamivu, amesema anafanya utafiti wa uchakataji wa tope choo kupata rasilimali gesi, mbolea ya mboji na maji taka kuwa safi ambayo hutumika kwaajili ya shughuli mbalimbali.
“Tunachukua maji taka na kuyasafisha ambapo baada ya hapo yanaweza kutumika kumwagilia mashamba na mimea kuwa safi kwa matumizi ya binadamu.” Amesema Ruhinda.
Aidha Ruhinda amesema gharama ya kusafirisha majitaka na kinyesi vyooni ni kubwa kutokana na ukosefu wa miundombinu ya kuhifadhia hivyo tafiti hizo zinafanyika kujaribu kuokoa hali hiyo.
Amebainisha kuwa hivi sasa kuna maeneo mawili tu ya kuhifadhia majitaka na kinyesi ya DAWASA maeneo ya Vingunguti na Kurasini pekee hivyo wanafanya tafiti kupata sehemu rahisi za kuhifadhia kuokoa gharama inayotumiwa kusafirisha.
“Watu hawapaswi kuwa na wasiwasi na majitaka yanayochakatwa kwasababu yanatumika sehemu mbalimbali duniani na yakishachakatwa hayawi na sumu yoyote yanakuwa salama kwa matumizi,” Amesema Ruhinda.