Watu watano wamefariki dunia kwa homa ya uti wa mgongo, kufuatia ugunduzi wa ugonjwa huo kwa watu 37 katika Wilaya ya afya ya Oti Sud, iliyopo eneo la Savannah, wakati wa kipindi cha Harmattan nchini Togo.
Waziri wa Afya wa Togo, Moustafa Mijiyawa amesema kati ya wagonjwa 37 waliotambuliwa, wengi wao ni watoto na watu wazima ambapo tahadhari imetolewa kupitia vyombo vya habari nchini humo ili kukumbusha dalili na mambo ya kuzingatia.
Amesema, “moja ya dalili ni homa, hasa ikiwa inakuja ghafla na yenye nguvu, maumivu ya kichwa, kutapika, shingo ambayo inakuwa ngumu na wakati mwingine usumbufu wa fahamu, wananchi wanapoona dalili mojawapo kati ya hizi ni vyema wakawahi kituo cha afya.”
Aidha, Mamlaka za afya nchini humo pia zimekumbusha raia wake hatua zinazopaswa kuchukuliwa, ili kukabiliana na kuenea kwa homa hiyo ya uti wa mgongo kwa kusisitiza watu kuepuka kukaa katika mazingira yenye vumbi, kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni, kulinda pua na midomo yao wakati wa kupiga chafya na kukohoa na kuwasiliana kwa karibu.