Rais John Magufuli leo Januari 17, ameungana na waumini wa kanisa katoliki la Bikira Maria Parokia ya Chato mkoani Geita kusali misa takatifu iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo, Padre Henry Mulinganisa.
Akitoa salamu katika misa hiyo, Rais Magufuli amewapongeza waumini wa kanisa hilo kwa kufanikisha upanuzi wa kanisa ambalo sasa lina nafasi ya kutosha waumini wengi zaidi kufanya Ibada kwa wakati mmoja.
Aidha ametoa wito kwa waumini hao na watanzania wote kuendelea kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka zake kwa Taifa na hasa kwa kuepusha janga la Corona nchini , ilihali ugonjwa huo ukiendelea kusababisha vifo vya maelfu ya watu katika nchi nyingine duniani.
Amesisitiza kuwa, kutokana na Tanzania kuepushwa na corona, Watanzania wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuchapa kazi zaidi hasa kuzalisha mazao mbalimbali yakiwemo ya chakula kwa ajili ya kuzisaidia nchi ambazo zinashindwa kufanya uzalishaji kutokana na watu wake kufungiwa majumbani na pia kukuza uchumi.
“Sasa hivi mvua zinanyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, nawaombeni sana ndugu zangu watanzania tulime mazao hasa ya chakula, tulime kwa wingi ili baadaye tuje kuwasaidia wenzetu ambao wanashindwa kulima kutokana na Corona.” amesemaRais Magufuli.