Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango anatarajiwa kuwaongoza wananchi wa Jiji la Dodoma kupanda miti ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo leo Januari 09, 2023 jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar yatakayofanyika Januari 12, 2023.
Dkt. Jafo amesema kuwa Makamu wa Rais ataongoza zoezi la upandaji miti katika maeneo ya Barabara ya Dodoma – Dar es Salaam, kuanzia Stendi kuu ya Dodoma (Nane nane) hadi Ihumwa pamoja na Shule ya Msingi Msalato.
Pia, amesema shughuli hiyo itatanguliwa na shughuli nyingine za upandaji miti Januari 10, 2023 katika maeneo ya pembezoni mwa barabara ya Dodoma – Dar es Salaam kuanzia chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) hadi Kilimo Kwanza ambayo itaongozwa na Waziri Dkt. Jafo.
Ameongeza kuwa Januari 11, 2023 zoezi la upandaji miti litaongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt Pindi Chana katika Bwawa la Swaswa wakati Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Sinyamule ataongoza zoezi hilo katika eneo la wazi la Chidachi.
“Mtakumbuka kuwa Serikali ilielekeza mwaka huu wa 2023 hakutakuwa na sherehe kubwa za maadhimisho ya Mapinduzi, katika Uwanja wa Amani kama ilivyozoeleka, badala yake gharama zilizopangwa kuadhimisha sherehe hizo zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imeazimia kudhimisha sherehe hizo kwa kuendeleza shughuli ya upandaji miti katika viunga na maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma,” amesema Jafo
Aidha, amewapongeza viongozi wa awamu zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika nyanja mbalimbali katika kuleta maendeleo endelevu kwa jamii ya pande zote za Muungano.
Akitoa pongeza kwa wadau mbalimbali Dkt. Jafo amesema shughuli za upandaji miti ni katika kuendeleza azma ya Serikali kuifanya Dodoma kuwa ya kijani inayopendeza na kuvutia huku akitoa wito wa kuyshiriki kwa pamoja.
Hivyo, amewataka Watanzania wote Bara na Zanzibar kupanda miti katika makazi yao na kuendelea kuitunza hadi ikue na kuongeza uoto wa asili katika nchi yetu.