Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu watatu kwa kosa la kumpeleka mtoto wa miaka (3) baa na kumnywesha pombe huku wakimchukua video na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Kamanda wa Polisi mkoani shinyanga ACP Debora Magiligimba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililofanyika katika baa ya bondeni kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo wilayani Kahama.
Aidha amesema kuwa jeshi la polisi linawashikilia watuhumiwa hao waliomdhalilisha na kumfanyia ukatili kwenye mitandao ya kijamii mtoto huyo kinyume cha haki ya mtoto kwa mujibu wa sheria ya haki ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009.
Watuhumiwa hao ambao ni Godius Katisha (32) mkazi wa Mwakitolyo ambaye ni baba mzazi wa mtoto huyo na mmiliki wa Bondeni baa, Alphonce Pima (32), na Oscar Makondo (35) mkazi wa mtaa wa Mayila Kahama.
Kamanda wa polisi Magiligimba amsema baada ya tukio hilo kusambaa katika mitandao ya kijamii kikosi kazi cha Askari wa uhalifu wa makosa ya kimitandao walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa.
Aidha ameitaka jamii kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vibaya ikiwemo katika maambukizi hatari ya virusi vya Corona ambapo amewatakaa wasitembee mitaani wala kuwapeleka kwenye mikusanyiko ya watu.