Serikali inatarajia kuandikisha Watoto wa elimu ya awali 1,877,484 wenye rika lengwa wakiwemo wavulana 934,560 na wasichana 942,924 na darasa la kwanza 1,729,180 wakiwemo wavulana 860,870 na wasichana 868,310 ifikapo Januari, 2024.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge jijini Dodoma.
Amesema, “Hadi sasa jumla ya watoto wa elimu ya awali 407,138 sawa na asilimia 21.7 wakiwemo wavulana 201,244 na wasichana 206,253 wameandikishwa. Kati ya watoto wa elimu ya awali, wenye mahitaji maalum walioandikishwa ni 960 kati yao wavulana ni 488 na wasichana ni 472.”
Majaliwa ameongeza kuwa, walioandikishwa kujiunga darasa la kwanza ni 593,452 sawa na asilimia 34.3 wakiwemo wavulana 293,728 na wasichana 299,724. “Kati ya wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa wenye mahitaji maalum ni 1,365 wakiwemo wavulana ni 733 na wasichana 632.”
Aidha, amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini wasimamie zoezi la uandikishaji katika maeneo yao jambo ambalo amesema itakuwa vema likihitimishwa Desemba 31, mwaka huu. “Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha wazazi na walezi wote wenye watoto wenye rika lengwa, wawaandikishe watoto hao ili waweze kuanza masomo ifikapo Januari, 2024.”