June 16, ni Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu, na umuhimu wa mtoto duniani.
Maadhimisho haya hufanywa tangu ilipotangazwa kuwa siku rasmi mwaka 1991 na jumuiya ya Umoja wa Afrika ambapo kauli mbiu ya Bara mwaka huu inasema “Tutekeleze ajenda 2040: Kwa Afrika inayolinda Haki za mtoto”
Chimbuko la maadhimisho haya ni azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini waliouawa tarehe 16 Juni, 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.
Itakumbukwa watoto hao walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu bora na hivyo kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi.
Kupitia Maadhimisho haya, Serikali na wadau tunakumbushwa kuandaa mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi, walezi na jamii kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto wa Afrika na kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha, maadhimisho haya ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa Sera za Taifa zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa kwa ujumla.
Kauli mbiu ya mwaka huu inawataka wazazi, walezi, Serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya mtoto ili aweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.