Watu saba wameripotiwa kuuawa wakati wa maandamano nchini Uganda baada ya kukamatwa kwa mgombea uraisi wa chama cha upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.
Maandamano hayo yalianza punde baada ya wafuasi hao wa Bobi Wine kupata taarifa ya kukamatwa kwa mgombea huyo wa upinzani siku ya Jumatano
Polisi wamethibitisha kuwa watu saba wameuawa wakati wa makabiliano kati yao na wafuasi wa Bobi Wine, na wengine 40 kujeruhiwa.
Taarifa ya polisi haikusema kuwa watu hao walifariki vipi ingawa video na picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa zinaonesha watu waliotapakaa damu huku wengine wakioneshwa kutoweza
kufanya lolote yaani wamepigwa risasi na kufariki Dunia.
Marekani imeshutumu ghasia zilizojitokeza katika mji mkuu wa Kampala na miji mingine nchini humo na kuzitaka pande zote kuchukua hatua za kupunguza wasiwasi uliotanda nchini humo.
Uganda inatarajia kufanya uchaguzi wa Urais mwezi Januari, 2021.