Watu kadhaa walioandamana dhidi ya polisi wameripotiwa kupigwa risasi na kuuawa huku wengine kadhaa wakiwa wamejeruhiwa mjini Lagos, Nigeria.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, wamesema kuwa wameona miili ipatayo 20 ikiwa imetapakaa na wengine 50 wamejeruhiwa baada ya wanajeshi kufyatua risasi.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, limesema kuwa polisi walilazimika kutumia risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya zaidi ya waandamanaji elfu moja waliokuwa wamekusanyika katika mji wa kibiashara wa Lagos, nchini Nigeria.
Shirika hilo limesema kuwa wana ushahidi tosha unaoonesha polisi wakitumia mabavu dhidi ya waandamanaji mjini Lagos na wana kwa mujibu wa msemaji wa Amnesty International Isa Sanusi, wana video inayoonesha polisi wakiwaua wananchi, hivyo wanajaribu kuhakiki ni wangapi.
Kutokana na mapigano ya risasi yanayoendelea, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton, amemtaka rais wa Nigeria Muhammadu Buhari kuacha kuwaua vijana.
Jana Jumanne kumetangazwa amri ya kutotembea usiku kwa muda wa masaa 24 katika mji wa Lagos ambao ni kitovu cha biashara Nigeria, wakati vurugu zikiongezeka katika maandamano ambayo yametikisa miji kadhaa nchini humo.
Jeshi la Nigeria hata hivyo limedai kuwa wanajeshi wake hawakuweko katika eneo hilo la maandamano Jumanne lakini serikali imesema itafanya uchunguzi dhidi ya tukio hilo.