Watu wanne wameripotiwa kuuawa nchini Sudan katika siku ya kwanza ya maandamano ya kitaifa ya kupinga utawala wa Kijeshi nchini humo.
Vikosi vya Usalama nchini Sudan viliwarushia mabomu ya machozi baridi na kutumia risasi halisi kuwatawanya waandamanaji hao katika mkuu wa nchi hiyo Khartoum.
Wanaharakati wameitisha maandamano ya kupinga utawala huo kuanzia Jumapili, siku kadhaa baada ya msako wa kijeshi uliosababisha vifo vya mamia ya watu katika mji mkuu wa Khartoum.
Aidha, Wafanyikazi kadhaa wa benki, Viwanja wa Ndege pamoja na wa shirika la umeme nchini humo walikamatwa kabla ya mgomo wa kitaifa wa kupinga utawala wa kijeshi, limedai kundi kuu la waandamanaji
Wanaharakati wa kupigania demokrasia nchini humo wanasema kuwa baraza la jeshi haliwezi kuaminiwa baada kuzuka kwa ghasia ambapo wafuasi wengi wa Upinzani waliuawa jijini Khartoum na wamekataa kufanya mazungumzo ya amani na viongozi wa baraza hilo.
Jeshi lilichukua uongozi baada ya kumng’oa madarakani kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo, Omar al-Bashir mwezi Aprili mwaka huu na kuahidi kurejesha utawala wa kiraia baada ya kipindi cha mpito.
Hata hivyo, mpaka sasa baraza la Kijeshi linalotawala nchi hiyo (TMC) halijatoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo.