Waziri Mkuu wa Jaamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kati ya Julai 2016 na Januari 2017, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya imekamata watu 11,303 ambao wanatuhumiwa kujihusisha na uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Majaliwa amesema hayo katika Kikao cha Kazi cha Mawaziri na Naibu Mawaziri kilichofanyika Machi 3, 2017 kwenye ukumbi wa mikutano wa Hazina mjini Dodoma chini ya uwenyekiti wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Amesema kati ya hao, watu 9,811, walikutwa na kesi za kujibu ambapo 9,174 wametiwa hatiani, 238 hawakukutwa na hatia na wengine 478 upelelezi wa kesi zao unaendelea. Pia alisema tangu Tume mpya iundwe Februari mwaka huu, jumla ya watuhumiwa 79 wametiwa mbaroni na uchunguzi wa kesi zao unaendelea.
“Wengi kati ya hao, wameshikwa na vithibitisho, ingawa uchunguzi wa kesi zao bado unaendelea. Na hawa ni wale waliokamatwa na dawa za viwandani kama heroine na cocaine. Hatujawaingiza wale waliokamatwa na mirungi au bangi. Bado mikoa inaendelea na kazi, na hii operesheni ni ya nchi nzima,” alisema.
Uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.
Tangu wakati huo Serikali zote ziliendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo.
Serikali ya awamu ya tano iliamua kuhamia Dodoma baada ya kuridhishwa na ujenzi wa miundombinu na maeneo ya kutolea huduma za kijamii kwa wageni na wenyeji.