Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amemwagiza Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba kuwasimamisha kazi Maafisa saba wa Ofisi za Madini za Mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa kutokana na kutokuwa waaminifu katika shughuli zao za usimamizi wa Sekta ya Madini katika maeneo yao.

Agizo hilo amelitoa Dkt. Biteko Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga alipokutana na Wafanyabiashara wa Madini wa Kanda ya Ziwa kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara hao.

Dkt, Doto Biteko amesema, kuna baadhi ya watumishi wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ambao sio waaminifu na wanajihusisha na udanganyifu kwenye biashara ya madini ikiwemo kuwapunguzia wachimbaji viwango vya ubora wa madini yao ili wajipatie fedha.

“Nichukue fursa hii kuwatadharisha Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa yote nchini kuhakikisha mnawafuatilia kwa karibu Maafisa wenu wanaoshirikiana na baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiwaibia wachimbaji wadogo wa madini kwa kupaka mafuta kwenye mashine ya kupimia ubora wa dhahabu na kusababisha kupata kiwango cha chini cha ubora wa madini ukilinganisha na uhalisia wa madini yenyewe,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko amesema, kumeibuka kwa kundi la baadhi ya wafanyabiashara wa madini ya dhahabu wanaojihusisha na vitendo vya kuwatapeli wafanyabiashara wa nje ya nchi kwa kuwaomba fedha ili wawanunulie madini lakini wanashindwa kufanya hivyo na kujificha kwenye kisingizio kuwa wanaumwa Uviko-19 baada ya kupewa fedha.

Dkt. Biteko amesema kuwa, kundi hilo limekuwa likipokea fedha za ununuzi wa madini kutoka kwa wafanyabiashara wa nje ya nchi na kupiga picha maboksi ya madini yaliyofungwa siri za Wizara ya Madini ambazo ni feki na kuwatumia kwa njia ya mitandao kuwa mzigo uko njiani, jambo ambalo sio kweli na wanapotumiwa fedha wanazima simu zao.

“Hivi karibu amekuja mzungu ofisini kwangu analia kutapeliwa dola za Kimarekani 800,000 sawa na kiasi cha shilingi bilioni 7.2, tulipompigia simu mhusika aliyepatiwa fedha hizo alirusha maneno na kusingizia kuwa anaumwa ugonjwa wa korona jambo ambalo sio kweli,”.

Simba SC yatamba kuichakaza KMC FC
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Disemba 22, 2021