Wakurugenzi na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Taifa, Kanda na Mikoa, wametakiwa kuwatia moyo na kuwahamasisha watumishi wa kada za afya kwenda kusoma maeneo yenye mahitaji ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi nchini.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mafunzo Wizara ya Afya Dkt. Saitore Laizer ameyasema hayo hii leo wakati wa kufunga kikao kazi cha kuandaa mpango wa mafunzo ya kipaumbele kwa mwaka 2023/ 2024.
Amesema, “zoezi hili ni muhimu sana kwenye taasisi zetu hivyo tunaporudi kwenye maeneo yetu tujitahidi kuwahamasisha watumishi wetu waende kujiendeleza kwenye maeneo yenye uhitaji ili tuendelee kuboresha na kutoa huduma bora kwa wananchi wetu.”
Aidha ameongeza kuwa, ufadhili wa masomo utatolewa kulingana na mahitaji yaliyopo katika kila hospitali hivyo mpango huo wa mafunzo utasaidia kuwa na watumishi wenye tija katika maeneo yote, kwani Serikali imeweza kuboresha huduma za afya kwa kununua vifaa tiba vya kisasa na kuboresha miundombinu ya hospitali zote za Mikoa, Kanda na Taifa.