Wauguzi na wakunga nchini wametakiwa kutumia lugha nzuri wanapokuwa wakiwahudumia wagonjwa kwani kutokufanya hivyo ni kinyume na maadili na miiko ya kazi yao.
Wito huo umetolewa na mkurugenzi wa uuguzi na ukunga kutoka wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ziada Sellah, wakati akiongea na wauguzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha-Mount Meru jijini Arusha.
“Vitendo hivi ni kinyume na maadili na miiko ya kazi yetu kwani katika viapo vya utumishi mliapa kuwatumikia na kuwahudumia wagonjwa kwa moyo na upendo, hivyo hakikisheni mnatimiza viapo vyenu,” amesema Ziada.
Aidha, Ziada amewapongeza wauguzi wote kwa kupambana vyema katika janga la Covid-19 na kusimama mstari wa mbele katika kupambana na ugonjwa huo kwani ugonjwa huo ni mpya na bado haujawa na chanjo wala tiba.
“Niwapongeze sana kwa mapambano dhidhi ya ugonjwa huo ambao uliikumba dunia na nchi yetu,licha ya mazingira hatarishi lakini mliweza kupambana na hatimaye ugonjwa kuondoka hapa nchini” amesema Ziada.
Wauguzi hao wametakiwa kutambua thamani yao kwa kuwa wao ni askari wa mbele katika vita zote za magonjwa, humpokea mgonjwa kwa mara ya kwanza anapofika kituo cha afya na kumuhudumia kipindi chote anapokuwepo hospitalini hapo.
Katika ziara hiyo Ziada alizindua kitabu kilichoitwa “COVID-19 VITA YA KARNE YA 19” kilichoandikwa na afisa muuguzi Jane Barakululiza wa hospitali hiyo ambacho kinaongelea maisha kipindi cha Corona na hata baada ya Corona.
Pia alitunuku zawadi kwa wauguzi waliopambana vyema katika kupambana na ugonjwa wa Corona.