Shirikisho la soka barani Afrika (CAF), kupitia kamati yake maalum ya kuzisaidia nchi tano zitakazoshiriki kwenye fainali za Kombe la dunia 2018 nchini Urusi, imekubaliana kuzipa nchi hizo dola za Kimarekani 500,000 kila moja.
Kamati hiyo iliyoundwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika Novemba 16, mwaka huu mjini Rabat, Morocco chini ya Makamu wa kwanza wa Rais wa CAF, Kwesi Nyantakyi, imeanza kufanya kazi yake kwa kuonyesha namna ilivyojizatiti katika harakati za kuziwezesha timu za Afrika kufanya vyema kimataifa.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, Kalusha Bwalya na Marais wa Vyama vya Soka vya nchi tano zilizofuzu Kombe la dunia mwakani imefikia hatua huyo baada ya kikao chake cha mjini Moscow, Urusi kuelekea upangaji wa ratiba ya Kombe la Dunia Desemba 1, 2017.
Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya maandalizi timu hizo kabla ya kuingia kwenye michuano ya kombe la dunia 2018 nchini Urusi.
Kamati ya maalum ya kuzisaidia nchi tano zitakazoshiriki fainali za Kombe la dunia 2018 nchini Urusi, pia itazisaidia vifaa vya michezo nchi hizo.
Katika fainali za kombe la dunia 2018 Afrika itawakilishwa na Misri, Morocco, Nigeria, Senegal na Tunisia.