Jumla ya Wawekezaji wapatao 23 kutoka nchi za Uganda, Kenya, India, Uturuki, China, Sudan, Falme za Kiarabu, Pakistan, Zambia na Tanzania waliotembelea kujionea maendeleo ya ujenzi wa Kongani ya Kisasa ya Viwanda iliyopo katika eneo la Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani wameonesha nia ya kuwekeza katika eneo hilo, endapo watathibitishiwa uwepo wa maji na umeme wa uhakika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Afriq Engineering and Construction anayehusika na usanifu na ujenzi wa miundombinu wezeshi katika kongani hiyo, Mhandisi Charles Bilinga amesema mradi huo unakusudia kutumia Dola za Marekani milioni 51, sawa ambazo ni sawa na shilingi bilioni 122.4 katika kipindi cha miaka mitano.
Kongani hiyo inakadiriwa kuwa na jumla ya viwanda 203 vyenye uwekezaji wa Dola za Marekani bilioni 1.326 sawa na Shilingi trilioni 3.182 ambapo kwa sehemu kubwa fedha hiyo inatarajiwa kutoka nje ya nchi na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na viwanda.
Amesema, “Kati ya wawekezaji 23 walioonesha nia ya kuwekeza, jumla ya wawekezaji watatu wako tayari kuanza ujenzi wa viwanda huku wakitarajia kuwa changamoto za maji na umeme zitatatuliwa haraka ambapo mmoja wa wawekezaji hao ni kutoka nchini Uturuki Tanturk Tanzania Power Company Limited ambae anatarajia kujenga kiwanda cha majenereta aina ya Perkins kwa ajili ya kuuza katika soko la Afrika Mashariki na Nchi za Kusini mwa Afrika.”
Mhandisi Bilinga amesema, ujenzi huo unatarajiwa kuanza Juni, 2023 na utagharimu takriban Shilingi bilioni 24 na unatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja 200 ambapo viwanda vingine vilivyothibitisha kuanza ujenzi ni kampuni kutoka nchini Uturuki ambayo itajenga kiwanda cha chuma kitakachogharimu Shilingi bilioni 36 na kutoa ajira za moja kwa moja 300 na kampuni nyingine ya Uturuki itajenga kiwanda cha mabati kitakachogharimu Shilingi bilioni 120 na kutoa ajira za moja kwa moja 300.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa Kongani hiyo kutoka kampuni ya Kamaka, Nelson Mollel amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha eneo la uwekezaji ambapo kasi hiyo ya ujenzi katika kongani hiyo umefanyika katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake na wanaendelea kuona matunda mema ya uwekezaji huo.