Katika harakati za kuyaongezea thamani na kukuza soko la Maziwa nje ya nchi, Serikali nchini imekutana na kufanya mazunguzo na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Ireland, wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta hiyo.
Akizungumza na wawekezaji hao jana, ofisini kwake katika mji wa Serikali uliopo Mtumba jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, amesema watu hao wanatoka Shirika la Sustainable Food Systems Ireland (SFSI).
Amesema kuongezwa kwa thamani ya Maziwa, kutaiwezesha Tanzania kuingia katika masoko ya nje ya nchi, yakiwemo ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ushirikiano na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Lengo la Wizara ni kuona tunapata soko na kuja kwa wadau wa namna hii inakuwa ni faraja na inagusa maisha ya mfugaji wa kawaida moja kwa moja, maziwa yatachakatwa, kuongezewa thamani na soko litakuwepo hivyo tungependa wafugaji wazalishe maziwa zaidi.” Amesema Prof. Gabriel.
Aidha amefafanua kuwa wizara ya mifugo na uvuvi inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inatengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji, ili soko la maziwa liendelee kuwepo kwani kwa sasa Tanzania inazalisha maziwa jumla ya lita Bilioni 2.7 kwa mwaka.
Akizingumza wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi wa shirika la SFSI, David Butler amesema wamekuwa wakifanya kazi katika nchi tofauti, na kufanya vizuri katika sekta ya nyama na maziwa kwa zaidi ya miaka 40, huku wakiendesha programu mbalimbali za kilimo, mifugo na kuyaongezea thamani mazao.
Butler ambaye ameambatana na Dkt. Seamus Crosse, kutoka Shirika la Greenfield International la Jamhuri ya Ireland, amesema watakutana na wataalam kadhaa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, ili kuangalia namna bora ya uwekezaji na uzalishaji wa maziwa nchini.
“Tutajadili mambo mbalimbali ya uwekezaji hasa katika sekta ya ufugaji eneo la uzalishaji wa maziwa kwa lengo la kuyaongeza thamani na kuyapatia soko sehemu mbalimbali,” Amefafanua Butler.