Wanawake wa chama cha mapinduzi (UWT) kutoka kata tatu za Njombe Mjini, Ramadhani na Mji Mwema, wamefanikiwa kufanya kongamano lao lililokuwa na lengo la kuhamasisha wanawake kushiriki na kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa,vitongoji na vijiji utakaofanyika tarehe 24 mwezi novemba mwaka huu.

Pamoja na kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi kongamano hilo lilitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Joseph Pombe Magufuli pamoja na serikali yake ya awamu ya tano kwa kutekeleza vema Ilani ya CCM.

Wakisoma risala mbele ya mgeni rasmi Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Njombe kupitia CCM Dkt, Susan Kolimba Wanawake hao walisema,

“Lengo kubwa kukumbushana kuhusu uchaguzi uliopo mbele yetu wa serikali za mitaa ili wanawake wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali pia kumshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya hakika amekijengea sifa chama cha mapinduzi” wamesema wanawake hao.

Kupitia risala hiyo wanawake hao walitoa azimio la kulaani ukatili wa kijinsia unaofanywa dhidi ya wanawake na watoto.

Akizungumza na wanawake hao, mgeni rasmi Dkt, Susan Kolimba, aliwapongeza kwa kuamua kufanya kongamano hilo lenye lengo la kutambua umuhimu wa kuhamasisha wanawake kushiriki na kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, na kutambua mchango mkubwa wa, Rais Magufuli katika kutekeleza vyema ilani ya chama cha mapinduzi ambapo miradi mikubwa ya vielelezo imeendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tunaona miradi mbalimbali ikitekelezwa katika Mkoa wetu ikiwemo ujenzi wa barabara ya Itoni Njombe Ludewa hadi Manda, Njombe Makete, ujenzi wa hospital kubwa ya Rufaa Njombe, vituo vya afya katika kata mbalimbali vimeboreshwa, uboreshwaji wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari katika mkoa wetu na miradi mingine mingi inayoendelea kutekelezwa” alisisitiza Dkt, Kolimba.

Aidha aliwapongeza pia kwa kuamua kutoa azimio la kulaani ukatili unaofanywa dhidi ya watoto na wanawake jambo ambalo ni moja ya changamoto kubwa hapa nchini sambamba na kuwaasa kuwa walinzi wa watoto na kutoa ushirikiano kwenye kamati za ustawi wa jamii zilizopo katika maeneo yao.

Kupitia kongamano hilo Dkt, Kolimba aliwataka wanawake wa UWT mkoani Njombe kujitokeza kwa wingi kushiriki na kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa kupitia chama cha mapinduzi pamoja na kuwashawishi wanachama wenye sifa wajitokeze kugombea nafasi hizo.

“Vita iliyoko mbele yetu ni ya kukipigania chama cha mapinduzi na kuhakikisha kwamba kinashinda na akina mama wote wenye sifa na uwezo wa kugombea uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa wanashinda ili uwepo wetu uweze kuonekana katika jamii” amesema Dkt, Susan Kolimba.

Baada ya kusikiliza baadhi ya changamoto zinazoikabili jumuiya ya UWT katika kata za Njombe Mjini, Ramadhani na Mjimwema Dkt, Kolimba amezijibu na kuzitatua changamoto hizo kwa kutoa vitendea kazi vya kiofisi ikiwemo katiba na kadi za wanachama wa UWT kwenye matawi yote ya kata hizo.

Akiendelea kujibu changamoto hizo ameahidi kutafuta mtaalamu kwaajili ya kutoa mafunzo ya ujasiriamali na uongozi kwa wanawake wa Kata hizo ambao walimweleza Dkt, Kolimba kuwa wangependa kupata elimu hizo.

Mbunge huyo wa viti maalumu mkoa wa Njombe Dkt, Susan Kolimba amewakabidhi fedha kiasi cha Tsh, milioni moja wanawake wa kata hizo tatu ili waweze kuendesha shughuli za kiuchumi katika maeneo yao kupitia vikundi vya akina mama huku akigawa kadi za UWT kwa wanachama wapya 22 waliojiunga na jumuiya hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM mkoa wa Njombe katibu wa UVCCM mkoani hapa Ndg, Amosi Kusakula amewataka wanawake kuhamasisha, kushiriki na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2020.

Wawekezaji wapanga mikakati kupandisha thamani na soko la Maziwa nchini
Serikali yasisitiza Nishati mbadala kuepuka uharibifu wa Mazingira.