Watu wawili wamefariki dunia na watatu kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko wa baruti kwenye mgodi wa madini ya Tanzanite wa kampuni ya California Camp uliopo katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Maresone Mwakyoma amesema tukio hilo limetokea jana Mei 7, 2021 saa 11 jioni katika kitalu B (Opec) kwenye mgodi huo unaomilikiwa na Deo Minja (48) mkazi wa Njiro jijini Arusha.
Amewataja waliofariki dunia kuwa ni Hamis Selemani na Issa Bakari na miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Mount Meru ya jijini Arusha na majeruhi ni Ismail Said, Jafari Naivasha na Rajabu Saidi waliofikishwa hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro lakini Rajab aliruhusiwa.
Mmoja kati ya wamiliki wa mgodi huo, Jerome Kilawe amesema ajali hiyo imetokea kwa bahati mbaya wakati shughuli zikiendelea.
Msimamizi mkuu wa njia iliyotokea ajali hiyo, Othman Miraji amesema hakuna uzembe uliofanyika bali ni bahati mbaya.
Rajab ambaye ni mmoja wa majeruhi amesema, “tulikuwa watano wakati ajali inatokea. Wakati ninakagua kazi mgodini nilimkuta mtaalamu wa milipuko anashindilia kwenye tundu moja, bahati mbaya baruti ikajikwaruza kwenye mwamba na kulipuka.”