Wazazi wa Kike wa Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Morocco wamepata Fursa ya kuingia katika Kasri la Mfalme Mohamed wa VI wa Morocco, ikiwa ni sehemu ya kupongezwa kwa Kikosi cha Timu ya Taifa hilo.
Morocco ilimaliza Nafasi ya Nne katika Fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizomalizika nchini Qatar Jumapili (Desemba 18), kwa Argentina kutwaa Ubingwa mbele ya Ufaransa.
Mashabiki wengi wa Soka wameonesha kufurahishwa na Picha ya pamoja iliyopigwa na kinamama hao, wakiwa na Wachezaji wa Morocco ambao baada ya kuwasili mjini Rabat walialikwa katika Kasri la Mfalme Mohamed VI.
Licha ya picha hiyo, baadhi ya Wazazi wa Kike wa Wachezaji wa Morocco waliongozana na Watoto wao nchini Qatar na walionekana kushangilia ushindi wa kila mchezo tangu Hatua ya Makundi.
Morocco iliyokua haipewi nafasi ya kufanya vizuri miongoni mwa Mataifa ya Afrika yaliyoshiriki Fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, ilicheza mchezo wa Mshindi wa Tatu dhidi ya Croatia na kupoteza kwa 2-1.
Kabla ya hapo Morocco iliishangaza Dunia kwa kuiondoa Hispania katika mchezo wa 16 Bora, kisha ikaifunga Ureno kwenye Hatua ya Robo Fainali kabla ya kukwama Hatua ya Nusu Fainali kwa kufungwa na Ufaransa mabao 2-0.
Kitendo hicho cha kupambana na kuweka Rekodi mpya na kuwa timu ya Kwanza ya Afrika kufika Hatua ya Nusu Fainali, kimekua chagizo kwa Mashabiki wa soka na Viongozi wa Serikali nchini Morocco kujitokeza kwa wingi kukilaki kikosi chao kilipowasili mjini Rabat.