Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameagiza Meneja wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza umeme cha Kinyerezi I, Ubungo I pamoja na Mhandisi Mkuu wa Kinyerezi II, Kinyerezi I, na Ubungo I, wasimamishwe kazi na wachunguzwe kwa uzembe.
Dkt.Kalemani ametoa maagizo hayo baada ya kubaini uzembe uliofanyika katika vituo hivyo wakati wa ziara yake Jijini Dar es Salaam, ya kukagua vituo hivyo na kuzungumza na Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
“Haiwezekani Meneja na Mhandisi Mkuu wote wasiwepo katika vituo vyenu vya kazi bila sababu za msingi, mitambo yote inafanyiwa ukarabati kwa wakati mmoja Hapana, hii haiwezekani ni uzembe wa hali ya juu lazima wachunguze na waondolewe katika nafasi zao za kazi”, amesema Dkt. Kalemani.
Aidha ametoa siku kumi na nne (14) kwa Bodi hiyo kuwafanyia uchunguzi mameneja na wahandisi wakuu hao na kumpatia majibu stahiki pamoja na kuiigazi Bodi ya TANESCO kuhakikisha kuwa mtaalamu wa kuunga kifaa cha kuongeza umeme(Buster) kilichopata hitilafu katika Kituo cha Kupoza umeme cha Kinyerenzi I, anapatikana na kufunga kifaa hicho ndani ya siku tatu (3).
Sambamba na hilo, amewataka wataalamu wanaofanya ukarabati katika vituo hivyo kufanya kazi hiyo usiku na mchana ili kukamilisha matengenezo hayo haraka, na vituo hivyo kuzalisha megawati zote za umeme unaotakiwa katika vituo husika.