Serikali imewaagiza Maafisa Mawasiliano kwa Umma kutoka Wizara na Taasisi za Serikali kuwa daraja muhimu kati ya serikali na wananchi, ili kuhabarisha shughuli za maendeleo zinazofanywa katika maeneo mbalimbali nchini.
Agizo hilo, limetolewa Mkoani Morogoro na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew wakati akifungua mkutano wa mwaka wa 107 wa mafunzo kwa wadau wa elimu kwa umma, na kusisitiza kuwa mafunzo hayo yatawaongezea uwezo wa kutekeleza majukumu hayo.
Mkutano huo, unajumuisha maafisa Habari wa Wizara, Taasisi na mashirika ya umma ukiandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kuandaa vipindi vya redio, Luninga na mitandao ya kijamii.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba alisema, wataendelea kutoa mafunzo hayo kwa kuwatumia wakufunzi waliobobea katika masuala mbalimbali ya upashanaji habari nchini.