Serikali imesema itahakikisha inashiriki kwenye pambano la Twaha Kassim ‘Twaha Kiduku’ na Abdalla Pazi ‘Dulla Mbabe’ linalotarajiwa kufanyika Julai, 24, Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi kwenye futari iliyoandaliwa na Mkurugenzi wa Peaktime Media Entertainment Limited, Seleman Semunyu.
Dk Abbasi akijibu ombi la Semunyu la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi katika pambano hili alisema atalifikisha na anaamini litakubaliwa maana pambano limepangwa kuchezwa tarehe nzuri.
“Serikali tutashiriki kwenye pambano hilo kwa sababu mchezo wa ngumi ni kati ya michezo inayoweza kuitangaza nchi kimataifa. Na kuanzia sasa kama timu inakwenda kuiwakilisha nchi isitarajie kukabidhiwa bendera tu bali itarajie na mengine maana tumetenga bajeti kwa timu za taifa,” alisema Dk Abbasi.